
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa katika Uwanja wa Mashujaa Jijini Dodoma leo Julai 25,2023 ambapo amesema mnara utakaojengwa katika uwanja huo wa Mashujaa utakuwa ni mnara mrefu zaidi Afrika.
“Siku ya leo ni siku ya tafakuri, sala na dua zaidi na sio siku ya kutoa hotuba, nitumie fursa hii kuiponngeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya RC Dodoma na Majeshi yetu kwa maandalizi mazuri, nimefurahi kwa mara ya kwanza maadhimisho yanafanyika katika uwanja mpya wa Mashujaa hapa Mji wa Serikali Mtumba ambapo hivi punde nimeuwekea jiwe la msingi”

“Kukamilika kwa uwanja huu wa Mashujaa kutaendelea kuongeza heshima na hadhi kwa Makao Makuu ya Nchi, nimeambiwa mnara uliopo ni wa mwaka huu, pengine mwakani tutakuja mwenye mnara wa kudumu ambao ujenzi wake unaendelea”
“Nilipofika nilioneshwa ramani uwanja utakavyokuwa nimevutiwa sana na ramani ya uwanja wa Mashujaa, uwanja huu utakuwa na migahawa ya Kimataifa, kumbi za mikutano na vivutio vingine vya Watu kupumzika na kupata burudani kubwa zaidi utakuwa na mnara mrefu kabisa ndani ya Afrika yetu labda ujengwe mwingine kabla wetu haujakamilika lakini ukianza kukamilika utakuwa mnara mrefu zaidi ndani ya Afrika.

“Naielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu na Wahusika wengine kusimamia ujenzi wa mnara na uwanja wa Mashujaa na miundombinu yote ikamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa, Wizara ya Fedha itoe fedha kwa kuzingatia mpango kazi wa ujenzi huu na kusiwe na ucheleweshaji”
Madina Mohammed