186 views 6 mins 0 comments

KENYA HALI TETE” WALINZI WA MAMA KENYATTA WAONDOLEWA

In KIMATAIFA
July 21, 2023

Nairobi. Hali ni tete nchini Kenya, huku watu saba wakidaiwa kupigwa risasi wakati wa maandamano yanayoendelea yakiongozwa na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga.

Taarifa zinasema watatu kati ya waliopigwa risasi ni katika Kaunti ya Nakuru, wawili Makueni na wengine wawili Migori.

Msimamizi wa hospitali iliyoko Migori, Oruba Ochere alithibitisha kuwa wanaume wawili waliojeruhiwa kwa risasi walipokewa kwa matibabu.


Wawili wapigwa risasi katika maandamano Kenya

Walinzi wa mama yake Kenyatta waondolewa


Ochere alisema mmoja amepigwa risasi kwenye paja na mwingine akipigwa mguuni.

Licha ya matukio ya watu kupigwa risasi, yamekuwapo matukio yanayoibua maswali, likiwemo la kuondolewa walinzi kwenye makazi ya Mama Ngina, mjane wa hayati Jomo Kenyatta. Mama Ngina ni mama mzazi wa Uhuru Kenyatta, Rais mstaafu wa Kenya.

Katika maandamano ya jana, waandamanaji walijitokeza maeneo mengi ya nchi na kusababisha shughuli kusimama, huku biashara zikidorora.



Shule zafungwa

Pia kutokana na maandamano hayo, Wizara ya Elimu na Wizara ya Usalama nchini Kenya ziliamuru kufungwa kwa shule za msingi na awali zilizopo katika majiji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu kuanzia jana Julai 19.

Kwa mujibu wa wizara hizo, shule zimefungwa kutokana na kupokewa taarifa za kiintelijensia za kiusalama, kwamba wahalifu wanapanga kuzua ghasia karibu na shule hizo.

“Kama hatua ya tahadhari ya kuhakikisha usalama wa watoto wa shule, imeamuliwa kwa shule za msingi na za sekondari zisalie kuwa zimefungwa,” imeeleza taarifa ya pamoja ya wizara hizo.

Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu na wa Usalama, Kithure Kindiki wameeleza katika taarifa kwamba watatangaza siku ambayo masomo yatarejea baada ya kutathimini hali ya usalama.



Mabalozi wacharuka

Mabalozi wa nchi mbalimbali wametoa tamko la kuwaonya Rais William Ruto na mpinzani wake, Odinga wakiwataka kuacha mara moja misimamo yao ambayo kimsingi inaumiza raia.

Mabalozi hao, wakiwemo wa Marekani na Uingereza, wanaamini Ruto na Odinga wakifanya hivyo watatatua mzozo unaoendelea na kuepusha maandamano ambayo yanagharimu maisha ya watu.

“Tunahuzunishwa na vifo na tuna hofu kuhusu viwango vya juu vya ghasia, ikiwemo matumizi ya risasi na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya majuzi,” imeeleza taarifa ya pamoja ya mabalozi hao.

Mabalozi wa Australia, Canada, Ujerumani, Denmark, Uholanzi, Uswizi, Ireland, Norway na Ukraine kwa pamoja walitia saini taarifa hiyo.

Onyo hilo limetolewa siku chache baada ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kulaani ghasia na maafa yaliyoshuhudiwa katika maandamano ya Jumatano wiki iliyopita.



Makazi ya Mama Ngina

Mama Ngina, mjane wa mwasisi wa Taifa hilo aliondolewa ulinzi Julai 18, baada ya kuwa wamewasili kwenye eneo lao la kazi.

Walinzi hao katika makazi ya Mama Ngina yaliyopo Gatundu, Kaunti ya Kiambu na Muthaiga jijini Nairobi, waliondoshwa jioni baada ya kuwasili eneo la kazi. Waliarifiwa kwamba wakaripoti vituo vya polisi vilivyopo jirani.

Vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya viliripoti taarifa hiyo, ikielezwa kwamba Mama Ngina hakupewa taarifa awali kuhusu kuondolewa kwa walinzi hao.

“Tuliondoa walinzi kwa ajili ya mazungumzo lakini watarejea. Ana haki ya kupata usalama,” ofisa mmoja wa polisi aliiambia tovuti ya The Star, huku akiomba kutotajwa jina.

Mama Ngina (90), mjane wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta kabla ya kuondolewa ulinzi alikuwa na jumla ya walinzi 30.



Aandamana na taulo

Katika hali ya kushangaza, mwanamume mmoja kutoka Kisumu alijitosa kuandamana akiwa na mwanawe wa kiume, mwenye miaka mitatu, wote wakiwa vifua wazi na taulo viunoni.

Mwanamume huyo, Victor Erick alionekana akitembea barabarani na mwanawe, huku akiwa ameshikilia bango.

“Huwa natoka natembea nikiwa nimevaa taulo, hata siku ya uchaguzi nilikuwa hivi, ndivyo ninavyopenda, sina wasiwasi wa kumleta mwanangu aandamane kwa sababu tuna amani, hatuna silaha,” alisema Erick alipozungumza na tovuti ya The Star.



Wasaidizi wa Odinga watekwa

Wasaidizi wawili wa Odinga wanadaiwa kukamatwa na polisi jana. Mkurugunzi wa Mawasiliano wa Chama cha ODM, Phillip Etale alitoa madai hayo katika taarifa iliyotolewa na chama hicho.

Waliotekwa ni msemaji wa Odinga, Dennis Onyango ambaye nyumba yake ilivamiwa na watu waliodaiwa ni polisi na kuondoka naye.

Polisi walikiri kufika katika nyumba ya msemaji huyo lakini hakuwapo.

Etale alisema mtoto wa Onyango alisema kwamba, watu hao walikwenda wakiwa na magari mawili waliyoyatumia kumtorosha baba yake.

“Polisi walivamia nyumba ya Onyango, kando mwa barabara ya Mbagathi na kumkamata. Mwanawe anasema waliondoka naye kwa magari mawili aina ya Subaru,” Etale alisema.

Etale alisema juhudi za kumpata Onyango hazikuzaa matunda, kwa kuwa hata walipojaribu kumtafuta kwa njia ya simu haikuwa hewani.

Mwingine ni Maurice Ogeta, ambaye pia ni mlinzi wa Odinga anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana wanaodaiwa pia ni maofisa wa polisi.

Inadaiwa watekaji walimshusha kwenye gari lake na kisha kumfunga na kumweka kwenye buti ya gari lake.

Baada ya dakika chache, inadaiwa watekaji walimtoa Ogeta kwenye buti na kumlazimisha kuwasaidia kuwasha gari hilo baada ya kuzimika.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram