WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika uwekezaji ili kuupiga jeki uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na walipa kodi wapya.
Hayo yamesemwa leo Julai 17, 2023 Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji, Tanzania Gilead Teri wakati wa mkutano wa kituo hicho na Jukwaa la Wahariri wa vyombo habari uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa kasi ya kukua kwa uwekezaji ni kubwa nchini kutokana na mazingira bora yanayowavutia wawekezaji hivyo kuwataka watanzania kuchangamkia fursa
“Mabadiliko ya sheria ya uwezekazaji Disemba 2022 yalileta sheria mpya ambayo imekuwa rafiki kwa wawekezaji kutoka Tanzania mazingira yanawabeba sana changamkieni hiyo nafasi ili kuufukuza umaskini”
“Watu watumie fursa zinazojitokeze Kutokana na kukua kwa uwekezaji ni lazima Watanzania wanufaike na uwekezaji huu” amesema Teri
Aidha Mkurugenzi huyo amesema miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa hapa nchini na wapo katika mkakati wa siku 1000 za kuipaisha zaidi sekta hiyo.
“Tuna mpango mkakati wa miaka mitatu, tukiwa na malengo ya kuongeza idadi ya wawekezaji tunataka kufikia mwaka 2026 tuvutie uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 5.” amesema Teri.
Kwa upande wake mjumbe wa Jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari Angella Akilimali amesema mkutano huo umewapa fursa ya kuyafahamu mengi kutoka kwenye kituo hicho na watauhabarisha Umma pamoja na kutoa elimu.
” Sisi tutahakikisha tunafuatilia ni nini ambacho wanafanya, kuyafahamu pia malengo ya serikali ni yapi kuhakikisha tunatangaza kwasababu fursa zipo nyingi lakini zisipotangazwa hakuna atakayezifahamu” amesema Angella
Mkutano huo ni tekelezo la Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu ambaye amezitaka taasisi na mashirika ya kiserikali kuwa na mikutano ya mara kwa mara hasa na jukwaa la wahariri ili kuyafahamu yale yanayofanywa na taasisi hizo.
Madina Mohammed