132 views 2 mins 0 comments

PPRA YAJIPANGA KUPUNGUZA SIKU ZA MCHAKATO WA UNUNUZI KUONGEZA UFANISI

In KITAIFA
July 17, 2023

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Eliakim Maswi wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema katika Mwaka wa Fedha 2023/24 imepanga kupunguza siku za mchakato wa ununuzi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kutekeleza miradi.

Hayo yamesemwa leo Julai 17,2023 jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Eliakim Maswi wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kubadilisha utendaji wetu kama mamlaka na anataka tutoke tulipo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo matumizi ya mifumo ya kielektroniki kuleta tija na ufanisi unaostahil,” amesema Bw.Maswi

Maswi amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga sh. bilioni 40.4 kwa PPRA kuendesha shughuli mbalimbali za kiutendaji.

Aidha amesema kuwa katika fedha hizo sh. bilioni 20 zitatumika kwa uwekezaji, ukaguzi wa taasisi na kuwajengea uwezo watumishi.

”Serikali imefanya maamuzi ya kuanzisha mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki National e-Procurement System of Tanzania (NeST) kudhibiti rushwa, mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi wa zabuni.”amesema

Hata hivyo amesema kuwa lengo la kuanzisha mfumo huo ni kuongeza uwazi katika ununuzi wa umma, usimamizi mzuri wa fedha za umma, kudhibiti vitendo vya rushwa, ufuatiliaji kukidhi sheria, uwajibikaji na udhibiti wa manunuzi.

Amesema kuwa tangu Julai Mosi mwaka huu mfumo wa NeST ulianza kutumika rasmi.

“Taasisi zinazosimiwa na Msajili wa Hazina na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, zinapaswa kuanza kutumia mfumo mpya kwa shughuli za ununuzi wa umma kuanzia mwaka huu wa fedha.

Ameongeza kuwa: “Ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu taasisi nunuzi zote za serikali hazitaweza kutuma mialiko ya zabuni katika mfumo wa zamani wa TANePS na badala yake zitapaswa kutumia mfumo wa NeST unaopatikana kwa kupitia anuani ya https://www.nest.go.tz,”

Pia amefafanua kuwa mamlaka haitasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria kwa wale wote watakaokiuka taratibu au watajihusisha na uovu wowote utakaoisababishia serikali hasara

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram