Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amesema mabasi 38 kampuni ya New Force Enteprises yamefutiwa ratiba za alfajiri ambapo mabasi 10 ni yale yanayoanza safari saa 9.00 alfajiri na mabasi 28 yanayoanza safari saa 11.00 alfajiri. Aidha, kuanzia tarehe 5 Julai, 2023, mabasi hayo yatafanya safari zao kuanzia saa 12.00 asubuhi na kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 3, 2023 katika Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, CPA Suluo amesema uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuwapo kwa uvunjaji wa Kanuni za Usafirishaji wa Magari ya Abiria, 2020 pamoja na matukio ya ajali ya mabasi hayo ambapo ndani ya takribani wiki nne; kati ya tarehe 6 Juni, 2023 na 2 Julai, 2023 mabasi ya kampuni ya New Force yamehusika katika ajali tano na sababu kubwa ni uzembe wa madereva wa mabasi hayo.
CPA Suluo ameongeza kuwa, uchunguzi wa awali uliofanywa na Mamlaka ulibaini kuwepo kwa uvunjaji wa makusudi wa Kanuni za Usafirishaji wa Magari ya Abiria, 2020 hususan kutumia ratiba za saa 9.00 alfajiri na saa 11.00 alfajiri zinazomtaka dereva anayeendesha basi la abiria kutumia kifaa cha utambuzi (i-button).
Vilevile amesema Kampuni ya New Force ni miongoni mwa watoa huduma waliopewa ratiba za saa 09.00 alfajiri na saa 11.00 alfajiri ambapo walipewa sharti la kuhakikisha madereva watakaondesha mabasi kwa ratiba hizo ni wale waliothibitishwa na LATRA na kupatiwa kitufe cha utambuzi (ibutton) ambapo wanapaswa kutumia kifaa hicho ili waweze kufuatiliwa kupitia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) pindi yanapokuwa safarini.
Naye Bw. Masumbuko Masuke, Meneja wa Kampuni ya New Force Enterprises amesema, “Tunafahamu hizi ajali zinagharimu maisha ya Watanzania pamoja na miundombinu iliyopo, tunaahidi kubadilika kwa kuwapeleka madereva wetu kufanya mtihani ili wathibitishwe na tutahakikisha tunawasimamia katika kufuata Sheria za Usalama Barabarani ili kuepusha ajali na hasara zinazojitokeza,”
Kwa upande wake, Bw. Leo Ngowi Katibu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA-CCC) amewataka abiria kupaza sauti zao na kutoa taarifa kwa Mamlaka husika (LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani) pindi wanapoona kuna vitendo hatarishi vinavyofanywa na dereva pindi wanapokuwa safarini na pia ameipongeza Mamlaka kwa hatua sahihi waliyochukua kwa kuwa inaonesha jinsi Mamlaka inavyojali watumia huduma na watoa huduma za usafiri ardhini
Madina Mohammed