289 views 3 mins 0 comments

Serikali yasaini mkataba na shirika la marekani (USAID)

In KITAIFA
June 23, 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) Balozi Samantha Power, mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gran Melia Jijini Arusha.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amesema serikali ya Marekani kupitia USAID imekuwa mdau muhimu katika kukamilisha juhudi mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania ya kijamii na kiuchumi katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, maji, usafi wa mazingira, kilimo, usalama wa chakula, maendeleo ya miundombinu, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora

“serikali ya Tanzania inathamini dhamira mpya ya USAID ya kusaini Mkataba mpya wa Malengo ya Maendeleo ya miaka mitano wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.1. ambapo mfumo huo wa makubaliano utasaidia juhudi za kuimarisha zaidi demokrasia, haki za binadamu na utawala, utoaji wa elimu na huduma za jamii pamoja na kuhusisha ukuaji wa uchumi”.Alisema Makamu mpango

Pia amesema kupitia ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani hususani Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) umesaidia kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo. Halikadhalika ushirikiano katika kupambana na Malaria kupitia Mpango wa Rais wa Marekani wa Malaria (PMI) umesaidia katika kupunguza ugonjwa nchini.

Aidha Makamu wa Rais ameipongeza USAID kwa kushikiana na Vodacom Tanzania kwa uanzishwaji wa Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama unaoenda sambamba na vipaumbele vya serikali katika kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Marekani ili kukuza zaidi uhusiano bora uliopo kwa manufaa ya nchi zote mbili na wananchi wake.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) Balozi Samantha Power amesema wanayo furaha kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali na kutambua hatua mbalimbali za maendeleo zinazofikiwa nchini Tanzania kama vile katika sekta za afya, ukuaji uchumi, kilimo na teknolojia.

Aidha ameipongeza Tanzania kwa kutekeleza vema Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama ambapo imekua kivutio kwa mataifa mengine ya Afrika kutaka kutekeleza mfumo huo.

Balozi Samatha amesema serikali ya Marekani kupitia USAID inatambua hatua zilizopigwa na Tanzania katika kuimarisha utawala bora, kukuza demokrasia, haki za binadamu pamoja na uhuru wa vyombo vya habari. Amesema dhumuni la serikali ya Tanzania la ukuaji wa kiuchumi linavyoenda sambamba na mageuzi ya kiserikali ikiwemo uwazi na uwajibikaji huharakisha maendeleo na kuvutia uwekezaji.

Shirika la Misaada la Marekani (USAID) limeongeza kiasi cha dola za Marekani milioni 5 katika kuunga mkono sekta ya kilimo nchini.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram