
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania, kutambua kuwa wananchi wana matumaini makubwa na uteuzi wao, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanakidhi matarajio yao na ya wadau wengine kwenye masuala ya sheria.
Akizungumza Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Othman amesema hayo wakati akiwasilisha mada katika Mafunzo Elekezi ya siku tano kwa Majaji wapya sita wa Mahakama hiyo na mmoja ambaye hakupatiwa mafunzo hapo awali, ambayo yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kilichopo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
“Watu mbalimbali huko nje wana matarajio makubwa na nyie, mtambue hilo, hivyo kafanyeni kazi zenu kwa uadilifu, jamii inawasubirini kwa hamu, maana nyie ni wapya,” amesema Jaji Mkuu Mstaafu Othman.
Aidha jaji Mkuu mstaafu Othman amewaambia Majaji hao kuwa wana majukumu mazito mbele yao, na kwamba ni wajibu wao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na umakini mkubwa.

Hata hivyo Mhe. Othman amewataka Majaji hao kutumikia majukumu yao mapya ya Mahakama hiyo katika namna itakayowafanya waache urithi mzuri kwa jamii.
“Mnatakiwa kuacha urithi(Legacy) katika Mahakama ya Rufani. Urithi katika maeneo mbalimbali, mathalani Jaji Mstaafu Mhe. Lewis Makame alikuwa akiandika hukumu zake kwa mtindo wa mashairi, uzuri yeye alisoma Kiingereza na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Makerere,” Akisisitiza Jaji Mkuu Mstaafu Othman.
Kwa upande mwingine Jaji Mkuu Mstaafu Chande amewahimiza Majaji hao kufanya kazi kwa kushirikiana ili kupata matokeo bora ya kazi.