
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi amesema ofisi yake haitosita kumchukulia hatua atakayebainika kukwamisha ujenzi wa shule za msingi na ukarabati wa madarasa kwani fedha za ujenzi na ukarabati huo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuboresha miundombinu ya elimu ya msingi.
Akizungumza ndejembi mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi katika Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Singida iliyolenga kukagua utekelezaji wa ujenzi wa shule za msingi na ukarabati wa madarasa kupitia mradi wa boost unaosimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI
” watakaobainika kukwamisha mradi huo watachukuliwa hatua kali ili iwe ni fundisho kwa wengine wenye nia ovu ya kukwamisha miradi yenye tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa”. Alisema ndejembi
Aidha Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati miradi yote ya ujenzi wa shule na ukarabati wa madarasa ili thamani ya fedha ionekane.
“Ninawaomba msimuangushe Mhe. Rais, hakikisheni mnakamilisha ujenzi ifikapo tarehe 30 Juni, 2023 kama ilivyopangwa ili kumpa nguvu Mhe Rais ya kuleta fedha nyingine”Alisisitiza ndejembi
Aidha Ndejembi amefafanua kuwa, Mhe. Rais ametoa bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi pamoja na ujenzi wa shule mpya kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa nchini, kitendo ambacho kinaonesha dhamira yake njema ya kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wilaya yake shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi wilayani kwake.
Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kwa kuwasisitiza Wakurugenzi Wote nchini na Wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari kuhakikisha wananunua vifaa vyote vya ujenzi vinavyohitajika kabla ya mwaka wa fedha kuisha ili miradi inayoendelea kutekelezwa iweze kukamilika kwa wakati.