Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki, na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu L. Nchemba, wameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya kusanifu Mradi Uendelezaji wa Mkoa wa Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP 2). Mradi huo unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Aprili 2024 utagharimu Shilingi Bilioni 800. Mikataba hiyo imesainiwa kati ya Ofisi ya TAMISEMI na Wakandarasi wanaosanifu mradi huo.
Waziri Kairuki amewataka Wakandarasi hao kuzingatia masharti ya mikataba yao na kuhakikisha kuwa hawatakuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa mradi huo. Amesisitiza kuwa ofisi yake itahakikisha utekelezaji wa mradi huo unakuwa na mafanikio makubwa na kuepuka dosari zilizojitokeza katika awamu iliyopita.
“Mradi huu unakwenda kutatua kero mbalimbali ikiwamo ujenzi holela wa makazi, miundombinu duni ya usafiri, mabadiliko ya tabia nchi kwa jiji la Dar es Salaam zinazosababisha mafuriko na utupaji taka ngumu ovyo,”amesema Kairuki
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba, ameongeza kuwa mradi huu umekuwa kilio kikubwa kwa wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakihoji kuhusu utekelezaji wake katika bajeti mbalimbali.
Maelezo ya mradi huo yaliyotolewa na Mratibu wa miradi ya serikali, Mhandisi Humphrey Kanyenye, yanaonyesha kuwa asilimia 74 ya fedha hizo zitatumika kwenye miundombinu ya barabara, mifereji, maeneo ya wazi, masoko, vituo vya mabasi, na kurekebisha miundombinu ya taka ngumu.