186 views 3 mins 0 comments

TANZANIA YADHAMIRIA KUBORESHA UHIFADHI WA URITHI WA UKOMBOZI

In KITAIFA
May 24, 2023

Ujumbe wa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja katika Kituo cha Makumbusho
ya Nelson Mandela Foundation Mei 23, 2023 Johannesburg Afrika Kusini.

Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
zimedhamiria kuboresha na kuimarisha uhifadhi wa urithi wa ukombozi kurithisha kizazi
cha sasa na vizazi vijavyo ili kuinua uchumi wa pande hizo mbili za Muungano.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyotumiwa na
wapigania uhuru wa Afrika Kusini Mei 23, 2023, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab
amesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zinahitaji kushirikiana ili kutunza urithi wake
kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

\"\"

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab (wa pili kushoto) akiwa akiwa na ujumbe kutoka tanzania wakitembelea Kituo cha Makumbusho cha Lilieseaf ambacho kilitumiwa na wapigania uhuru wa ANC Mei 23, 2023 Johannesburg Afrika Kusini.

“Tumekuja kujifunza namna wenzetu wanavyotunza na kuhifadhi urithi wa Ukombozi wa
nchi yao na namna wanavyotunza urithi huo ili na sisi tukaboreshe maeneo yetu ya
Ukombozi yaliyopo nchini kwetu’,

‘Wenzetu wamejitahidi kuweka vizuri historia yao ambayo haitaisha milele, ni kitu cha
kujivunia kwa upande wao, na sisi tuna mambo mengi ya kufanya kwa viongozi wetu
waasisi Mwl. Julius Nyerere na Abeid Aman Karume ambao kwetu ni urithi
usiosahaulika milele kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo” amesema Bi Fatma.

\"\"

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab (wa kwanza kulia) akisikiliza maelezo kuhusu Kituo cha Makumbusho ya Nelson Mandela Foundation kutoka Mkurugenzi wa Makumbusho hayo Bi Razia Saleh (wa kwanza kulia) Mei 23, 2023 Johannesburg Afrika Kusini

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Kituo cha Makumbusho cha
Liliesleaf, Bw. Mosima Tokyo Sexwale amesema msaada uliotolewa na Tanzania chini
ya Uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere katika ukombozi wa Afrika Kusini
hautasahaulika kamwe.

“Kiukweli, misaada ya hali na tuliyopata kutoka Tanzania wakati huo ikijulikana kama
Tanganyika hasa kipindi ambacho Madiba, Nelson Mandela akiwa bado anafanya
harakati za ukombozi chini kwa chini, tuliomba msaada wa kisiasa, lakini tulipata zaidi
ya misaada ya hali na mali pamoja na msaada wa kidiplomasia” amesema Mosima.

\"\"

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab (katikati) akisalimiana na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Kituo cha Makumbusho cha Liliesleaf, Bw. Mosima Tokyo Sexwale (kushoto) Mei 23, 2023 Johannesburg Afrika Kusini. Kulia ni Dkt. Resani Mnata, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni (Lugha) kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mafunzo hayo ni ya siku saba kuanzia Mei 21- 27, 2023 ambapo katika siku ya pili
ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Watendaji Wakuu wa Wizara hizo wamefanya
ziara Johannesburg katika vituo vya Taasisi ya Makumbusho ya Nelson Mandela
Foundation, kituo cha Makumbusho cha Lilieseaf ambacho kilitumiwa na wapigania
uhuru wa ANC pamoja na Makumbusho yanajulikana kama Constitution Hill eneo
ambalo linautajiri mkubwa wa namna mahakama zilivyofanyakazi wakati wa ubaguzi wa
rangi pamoja na magereza kwa wafungwa ambao walihukumiwa kwa kesi mbalimbali.