209 views 31 secs 0 comments

TANZANIA KUOMBA KUWA MWENYEJI WA MASHINDANO YA AFCON MWAKA 2027

In KITAIFA
May 24, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kushirikiana na Kenya na Uganda kupitia Pamoja Bid wamedhamiria kuwa
mwenyeji wa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (African Cup of
Nations) 2027.
Rais Samia amesema nchi hizo zinawania nafasi hiyo kwa kutambua mafanikio
makubwa ambayo Sekta ya Michezo imepata, hivyo kuwa wenyeji wa AFCON 2027
kutaongeza hamasa zaidi kwa ukuaji wa michezo hususan soka.
Aidha, Rais Samia amesema michuano hii itachangia katika ukuaji wa utalii kwa
kuwa ni mashindano ambayo hutazamwa na zaidi ya watu bilioni moja Barani Afrika
na maeneo mengi duniani kwa ujumla.
Vile vile, Rais Samia amesema mashindano hayo yataleta watu mashuhuri nchini
wenye ushawishi duniani hivyo huwezesha na kunufaisha sekta nyingi za uchumi
ambapo huchangia ajira, mapato kwa wafanyabiashara na serikali.
Kwa upande mwingine Rais Samia amesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni
Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania,
imeshafanya utafiti na kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa maandalizi ya
kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Mashindano ya AFCON yataweka rekodi kwa mara ya kwanza kufanyika katika
Ukanda wa Afrika Mashariki tangu yalipoanzishwa rasmi mwaka 1957.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu