332 views 3 mins 0 comments

12 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUFANYA VURUGU

In KITAIFA
May 23, 2023

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watuhumiwa 12 kwa tuhuma za
kufanya vurugu pamoja na uharibifu wa vitu mbalimbali na kupelekea mtu
mmoja kufariki dunia.
Akitoa taarifa hiyo leo Mei 22, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
ACP Justine Masejo amesema mei 22, 2023 muda wa saa 5:40 asubuhi
huko katika Kitongoji cha Magomeni kijiji cha Jangwani eneo la Mto wa
Mbu Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha, Askari wa hifadhi ya Manyara
wakiwa katika doria ya kawaida eneo la ziwa Manyara walikamata Wavuvi
watatu waliokuwa wakivua samaki katika maeneo yaliyozuiliwa kwa
uhifadhi.
ACP Masejo amebainisha kuwa mara baada ya kukamatwa kwa wavuvi
hayo, walijitokeza wavuvi wengine na kuzusha vurugu iliyopelekea askari
hao wa uhifadhi kushindwa kuwachukua watuhumiwa hao na kwenda
kutoa taarifa katika kituo cha Polisi.
Kamanda Masejo ameendelea kufafanua kuwa umati wa watu hao
walikwenda hadi kwenye ofisi ya kijiji cha Jangwani na kufanya uharibifu
mkubwa katika ofisi hiyo ya serikali kwa kuvunja madirisha pamoja na
kuchana bendera ya Taifa na kuondoka nayo kwa madai kuwa wavuvi
wenzao wamezamishwa maji wakati wanakamatwa na Askari wa uhifadhi.
Aidha baada ya uharibifu huo, kundi hilo liliamua kuelekea ofisi na makazi
ya Askari wa TANAPA yaliyopo Mto wa Mbu, lakini wakati wakiwa njiani
walivamia ofisi na makazi ya Askari wa TANAPA na kufanya uharibifu
mkubwa wa magari kwa kutumia marungu na mawe pamoja na kupanga
mawe barabarani kuzuia watumiaji wengine wa barabara wasiendelee na
shughuli zao.
ACP Masejo amebainisha kuwa licha ya juhudi za kuwazuia kuingia katika
ofisi na makazi hayo ya Askari wa TANAPA watu hao waliendelea
kupambana na askari wa uhifadhi na ndipo jeshi la Polisi waliongeza nguvu

kuokoa na kuzuia madhara zaidi kwa binadamu na mali za watu binafsi na
za serikali.
Aliendelea kueleza kuwa kutokana na ghasia hizo mtu mmoja alipoteza
maisha na watu wengine saba walijeruhiwa na wamelazwa hospitali
wakiendelea na matibabu.
ACP Masejo amesema upelelezi wa shauri hilo unaendelea ili kubaini
walioanzisha na kushiriki katika vurugu hizo pamoja na kuchunguza madai
ya wananchi kuhusiana na wavuvi waliozamishwa katika maji.
Sambamba na hilo uchunguzi ukibaini ukweli kulingana na ushahidi watu
hao watafikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linatoa onyo kali kwa baadhi ya watu ambao
wanatabia ya kupambana na vyombo vya dola ambao kimsingi wamepewa
dhamana ya kulinda maisha ya watu, mali zao pamoja usalama wa nchi
kwani inaweza kusababisha madhara makubwa.
Lakini pia jeshi hilo limesema endapo kuna changamoto yoyote zipo
taratibu nzuri za kufuata kuliko kufanya vurugu na kujichukukulia sheria
mikononi kwa kupambana na vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria ya
kulinda maisha ya watu, mali zao na rasilimali za Taifa.