180 views 55 secs 0 comments

UJENZI DARAJA LA WAMI WAKAMILIKA, JPM WAFIKIA 72%

In KITAIFA
May 22, 2023

Serikali imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23, miradi ya barabara
kuu iliyopangwa kutekelezwa ni ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara
zenye urefu wa kilometa 470 pamoja na ukarabati kwa kiwango cha lami wa
barabara zenye urefu wa kilometa 33.

Aidha, kazi nyingine ni kuendelea na ujenzi wa madaraja makubwa matatu
ambayo ni Daraja la JPM (Kigongo – Busisi, Mwanza), Daraja la Pangani
(Tanga) na daraja la Wami (Pwani).

\"\"

Vilevile, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilipanga kuanza ujenzi
wa madaraja saba ambayo ni Godegode (Dodoma), Sukuma (Mwanza),
Mirumba (Katavi), Simiyu (Mwanza), Sanza (Singida), Mkenda (Ruvuma) na
Mpiji Chini (Dar es Salaam).

Pia, Serikali ilipanga kuanza ukarabati wa daraja moja la Kirumi pamoja na
kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa madaraja sita.

Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,
Mhe. Prof. Makame Mbarawa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2023/24.

“Hadi Aprili, 2023, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa
kilometa 179.18 umekamilika na ujenzi wa kilometa 290.82 unaendelea ambapo
kilometa 161.49 za tabaka la juu la msingi (basecourse), kilometa 192.03 za
tabaka la kati la msingi (Sub – Base) na kilometa 259.94 za tuta la barabara
zimejengwa,\” amesema Prof. Mbarawa.

Amefafanua kuwa, “Ujenzi wa daraja la Wami umekamilika, ujenzi wa
madaraja mawili ya JPM (Kigongo – Busisi, Mwanza) umefikia asilimia 72 na
kwa daraja la Pangani (Tanga) ujenzi umeanza na umefikia asilimia 3. Aidha,

manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mengine sita yapo
kwenye hatua mbalimbali”.