198 views 2 mins 0 comments

RAIS SAMIA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI UJENZI WA MINARA 758

In KITAIFA
May 13, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa
wito kwa Makampuni ya simu kubuni teknolojia ya gharama nafuu itakayowezesha
kila Mtanzania kupata huduma ya mawasiliano popote alipo nchini.

Rais Samia ametoa wito huo leo wakati wa utiaji saini mikataba ya upelekaji huduma
za mawasiliano nchini kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na watoa
huduma za mawasiliano uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.

\"\"

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Viongozi wengine wakati akishuhudia utiaji saini Mikataba ya kupeleka Huduma za Mawasiliano Vijijini kati ya Serikali na Makampuni ya Simu (TTCL, Vodacom, Airtel, Halotel, Tigo) iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 13 Mei, 2023

Aidha, Rais Samia ameyataka Makampuni hayo kuleta teknolojia inayoendana na
mazingira ya Tanzania kwa kuwa zipo changamoto zinazotokana na hali ya
kijiografia na kipato kidogo cha wananchi katika baadhi ya maeneo.
Rais Samia pia amewataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA)
kushirikiana na UCSAF na wakandarasi kuhakikisha njia zinapitika katika maeneo ya
vijijini inapokwenda kujengwa minara hiyo.
Hali kadhalika, Rais Samia amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha
kuwa minara inayokwenda kujengwa vijijini inapelekewa umeme ili faida
inayokusudiwa ipatikane haraka.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema kuwepo kwa huduma bora za
mawasiliano hususan katika maeneo ya vijijini ni muhimu sana kiuchumi, kisiasa,
kijamii, kiutamaduni na hata katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi yetu.

Miradi miwili iliyotiwa saini ni ya ujenzi wa minara 758 katika Kata 713 wenye
gharama ya Shilingi bilioni 265.3 pamoja na mradi wa kuongeza uwezo wa minara
304 ya mawasiliano utakaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 10.2.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu